Uamsho na Matengenezo - 3

 

 

SOMO LA TANO.

UDANGANYIFU NA MIUJIZA YA SHETANI YA SIKU ZA MWISHO.

Imeandaliwa na Mch. Filbert J. Mwanga

 

FUNGU KUU: UFUNUO 13:13, 14; 16:13, 14.

UTANGULIZI

Ulimwengu mzima sasa umeingia katika zahama kubwa sana ya kushindwa kutambua utendaji halisi wa Roho wa Mungu katika maisha ya watu. Wengi wamechanganyikiwa na jina la Yesu kutumiwa katika miujiza na mambo ya ajabu na kutisha yanayotokea duniani. Kwa kadiri tunavyofikia mwisho wa wakati tunaona roho bandia nyingi zinatokea na kutenda miujiza jambo ambalo linawachanganya wakristo wa kweli na kuwadumaza wanadamu washindwe kumtafuta Mungu katika ukweli wake. Shetani amekamata usukani wake sawa sawa akijua kuwa ana muda mchache tu hapa duniani kiasi ya kwamba hakuna anayemuona dereva huyu wa kupeleka watu Jehanamu huku akiongoza gari lake vyema katika barabara yake. Utendaji wake umefichwa katika vazi la Ukristo jambo ambalo itakuwa vigumu sana kwa watu kuling’amua. La kushangaza makanisa yote amevamia na imani kubwa duniani zote anaziongoza katika udanganyifu wake. Na hivyo sio salama kujenga imani katika miujiza ya wachungaji, viongozi, ama wafuasi wa dini kama ndicho kipimo pekee cha kumtambua mtu anayeongozwa na Roho Mtakatifu. Mama White anasema kuwa:

“Mwendee Mungu wewe binafsi, omba upate kuangaziwa na nuru ya mbinguni, ili uweze kuujua ukweli, ili kwamba adui atakapoleta maonyesho ya ajabu wakati adui atakapokuja kama malaika wa nuru, uweze kutofautisha kati ya utendaji wa kweli wa Mungu na kazi ya uigizaji bandia wa nguvu za giza…. Watu wa Mungu hawatakuwa salama kwa njia ya kutenda miujiza kwa maana Shetani ataigiza muujiza watakayoifanya.” (3SM 389 (1888); 9T 16 (1919).

Kwa kuwa watu wamekabiliwa na matatizo makubwa ya magonjwa, umaskini, na hata nguvu za giza. Shetani atatumia njia hiyo hiyo katika udanganyifu wake akidai kuwa anawapatia ahueni kumbe sivyo ilivyo zaidi ya yote anawaingiza katika maumivu makali zaidi kwani baada ya kuwapa ahueni ya muda kitambo anawatosa katika lindi la upotevu kwa kuwafanya kuwa watumwa wake. Mama White anasema wazi: “Namna ambavyo kwayo Kristo alitenda kazi ilikuwa ni kulihubiri Neno, na kuwapa ahueni wenye kutaabika kwa kufanya miujiza ya uponyaji. Lakini nimeelekezwa kuwa hatuwezi sasa kutenda kazi kwa namna hii, kwa maana Shetani atatumia uwezo wake kutenda miujiza. Watumishi wa Mungu leo hawawezi kufanya kazi ya Mungu kwa njia ya miujiza. Kwa sababu matendo bandia ya uponyaji, yakidaiwa kuwa yametoka mbinguni, yatafanywa.” (2 SM (1904).

Hili halimaanishi kuwa Wakristo wa kweli hawatafanya miujiza kabisa bali tahadhari inayotolewa ni kuwa muujiza usitegemewe kabisa katika swala la kuthibitisha imani ya kweli. Miujiza itatumika saa ya mwisho katika kufunga kazi ya injili kama ilivyohusika katika ufunguaji wa kazi ya injili. Hiki ndicho Biblia inaposema dunia itaangazwa kwa utukufu Wake.

 

SOMO

Mambo yanavyoendelea sasa ni kuwa wachungaji na wakristo wengi wamefika mahali wameshindwa kuthibitisha Ukristo wa kweli badala yake wanahitaji kuuthibitisha kwa kutumia wale wote wanaotenda miujiza. Unaweza ukaona kuwa waumini wengi leo wanafurika mahali ambapo matangazo yamebandikwa kuwa kutakuwa na uponyaji na hata miujiza kutendaka. Tumeona baadhi ya Waadventista Wasabato wakitoka na kuliacha kanisa kwa kigezo kuwa hakuna Roho wa Mungu eti kwa sababu ibada zetu zimepoa, hakuna uponyaji na miujiza. Hivyo

ndivyo wanavyofikiri kuwa utendaji wa Mungu unathibitishwa kwa njia hizo za shamrashamra na misisimko katika ibada. Watu wanaacha Biblia kando ambayo kwa hakika ndiyo pekee na kipimo cha pekee cha kuthibitisha Ukristo wa Kweli na Ukristo bandia. Mama White anasema:

“Kama wale wanaofanya miujiza kwa njia ya uponyaji wanapata heshima na umashuhuri kwa njia ya miujiza wanayoifanya na kwa njia hiyo kuipuuza sheria ya Mungu na kuendelea katika kutotii, ingawa wana uwezo kufanya hili na kwa kiwango hicho, haina maana kuwa wana uwezo mkuu wa Mungu. Kinyume chake ni kwamba wanafanya miujiza kwa uwezo wa Yule mdanganyifu mkuu.” – 2SM 50, 51 (1885).

“Kamwe nafasi ya Biblia haiwezi kuchukuliwa na matendo ya miujiza yapasa kweli hizi zifunzwe na kuchunguzwa; lazima itafutwe kama hazina iliyositirika. Kuna mianga ya ajabu ndani yake ambayo haiwezi kupatikana popote kando ya Neno la Mungu, na hakuna kitu chochote kinachoweza kuchukua nafasi yake. Lishikilie Neno na uling’ang’anie, lipokee Neno lililosimikwa imara ambalo linawafanya watu kuwa na hekima na hatimaye wapate wokovu.” 2SM 48 (1894).

 

Jambo la kusikitisha ni kuwa hata ndani ya kanisa baadhi ya washiriki wamefika mahali wanachanganyikiwa na uponyaji huu bandia. Unapotazama television agenda kubwa ni tangazo la uponyaji na miujiza inayotendeka duniani kwa jina la Yesu. Wengi wanafikiri Shetani hawezi kufanya miujiza na mambo ya kushangaza kama hayo kupitia wale wanaoitwa wachungaji. Waadventista Wasabato wamepewa kila kitu kupitia vitabu vya roho ya unabii lakini bado wengi wanajaribiwa na mambo hayo. Mama White anasema kuwa:

“ … Neno la Mungu linatangaza kwamba Shetani atatenda miujiza. Atawafanya watu kuwa wagonjwa, na kisha kwa ghafula ataondoa kwao uwezo wake wa Kishetani. Ndipo watu hawa watafikiriwa kuwa wameponywa. Matendo hayo ya uponyaji unaoonekana yatawatia Waadventista wa Sabato katika Jaribio. (2SM 53)…. Chini ya uongozi wa pepo hao wachafu, watu watafanya miujiza. Watawafanya watu kuwa wagonjwa kwa kuwatupia uchawi, kisha watauondoa, na kuwafanya watu wengine kusema kwamba wale waliokuwa wagonjwa wameponywa kimiujiza. Jambo hilo Shetani amelifanya tena na tena.” (2 SM 53).

Mojawapo ya kitu cha kushangaza kinachosumbua wengi ni pale wanapohoji swala la utendaji wa wa mtu mmoja anayeitwa T.B. Joshua (wa Emmanuel TV). Maneno yake yanaonekana yamejaa hekima, busara, mvuto, miujiza ya kutisha mpaka wazungu wanatoka pande zote duniani kuja Nigeria. Anatoa misaada ya chakula na fedha kwa wajane na yatima na hata watu wasio na uwezo. Jambo ambalo linaonyesha hajaanzisha kanisa kwa ajili ya njaa au fedha. Lakini angalia hili ambalo Mama White alipoonyeshwa watu wa jinsi hii:

“Akiwa amejigeuza kama malaika wa nuru, atatembea hapa duniani kama mtenda maajabu; kwa lugha tamu atatoa maoni ya hali ya juu. Maneno mazuri yatasemwa naye na matendo mazuri yatatendwa naye. Kristo atakuwa ameigizwa kabisa kimaumbile, lakini katika jambo moja itakuwapo tofauti kubwa sana. Shetani atawageuza watu wasitii sheria ya Mungu. Licha ya hayo, ataigiza haki kwa uzuri sana, kiasi kwamba kama ingaliwezekana, angeweza kuwadanganya hata walio wateule. Wafalme, marais, watawala katika ngazi za juu, watakubaliana na nadharia zake potofu.” (FE 471, 472).

Mara nyingi watu wamekuwa rahisi kuamini kuwa kila mtu anayedai kuwa anaongozwa na Roho Mtakatifu ni mkweli. Biblia inaweka bayana kuwa ni muhimu sana kuzijaribu hizo roho. Unaposoma 1 YOHANA 4:1 – Yohana anasema zijaribu hizo roho sio kuamini kila roho. Hata ndani ya kanisa zile nyota tunazozishangilia kwa ujuzi wa hekima ama maneno yao mazuri itakuwa ni hatari sana kuwatumainia watu kama hao. Mama White anasema kuwa, “Nyota nyingi ambazo tulikuwa tunaziheshimu na kuzishangilia kwa sababu ya mng’ao wake zitazimika na kuwa giza” – PK 188 (1914).

MWITO

Usalama wangu kama mkristo katika kipindi hiki cha mwisho katika kuyapinga majaribu ya Shetani ni kusimama katika kweli ya Neno la Mungu. Yesu alisema watu wa Mungu watakuwa wametambulika kwa ile KWELI! (Yohana 17:17). Hatutakaswi na miujiza. Pambano kuu la Mwisho litakuja kati ya wema na uovu, Kristo na Shetani. Yesu atatenda miujiza na Shetani pia. Mama White anasema kuwa: “Katika njozi za usiku picha zilipita mbele yangu za vuguvugu kuu la matengenezo miongoni mwa watu wa Mungu. Wengi walikuwa wakimsifu Mungu. Wagonjwa waliponywa, na miujiza mingine ilitendeka. Roho ya maombezi ilionekana, kama vile ilivyodhihirika kabla ya siku ile kuu ya Pentekoste. Mamia kwa maelfu walionekana wakizitembelea familia, na kufungua mbele yao neno la Mungu. Mioyo ilisadikishwa kwa uweza wa Roho Mtakatifu, na roho ya uongofu wa kweli ilionekana. Kila upande milango ilifunguliwa kwa ajili ya kuutangaza ukweli. Ulimwengu ulionekana kuangazwa na mvuto kutoka mbinguni. Mibaraka mikubwa ilipokewa na watu wa Mungu walio wa kweli na wanyenyekevu.” (9T 126).

Ni kazi ya adui kuwaletea watu mashaka kwa kutoamini ukweli mara tu wanapoamini. Tunaweza kumwona mtu ndani ya kanisa akiingia na kuonyesha msimamo mzuri wa roho ya kutaka kujifunza lakini adui hatimaye anapanda magugu ya kutoamini taratibu za kanisa kwani sasa anajiamini kuwa ni mjuzi wa neno la Mungu. Mama White anasema wazi kuwa,

“Ni mpango wa Shetani kudhoofisha imani ya watu wa Mungu kuhusu Shuhuda. Halafu hufuata kuonea mashaka maswala muhimu ya imani, nguzo za msimamo wetu, halafu kuyaonea mashaka Maandiko Matakatifu na ndipo hujongea taratibu kuelekea upotevuni. Wakati shuhuda ambazo hapo kwanza ziliaminiwa, zinapoonewa mashaka, na kutupiliwa mbali, Shetani anajua kuwa wale waliodanganyika hawatakomea hapa tu, kisha huongeza juhudi zake maradufu mpaka amewatosa kwenye uasi wa wazi, ambao huwa kitu kisichotibika na kuisha katika uangamivu.” (4T 211).

 

Tunaishi kipindi cha mwisho ambacho hata Yesu alimuona Shetani akiudanganya ulimwengu na miujiza hii itawachanganya hata wateule. Kipindi cha dhiki ambayo Bwana asipoingilia kati kwa wateule itakuwa ni hatari ya kutisha (MATHAYO 24:22 -24). Usalama kwa watu wa Mungu utakuwa ni kuwa chini ya miguu ya Yesu wala sio ujuzi wetu. Mama White anasema hivi “Nendeni kwa Mungu ninyi wenyewe, ombeni kwamba mpate kuelimishwa na mbingu, ili mpate kujua hakika ya kwamba mnaujua ukweli, ili kwamba wakati uwezo wa Shetani ufanyao miujiza ya ajabu utakapodhihirishwa, na huyo adui kuja kama malaika wa nuru, muweze kubainisha kati ya matendo ya kweli ya Mungu na matendo ya kuigiza ya nguvu za giza” (RH Extra 24/12/1889).

 

 

 

 

SOMO LA SITA.

UMWAGWAJI MKUU WA MVUA YA MASIKA – ROHO MTAKATIFU!

Imeandaliwa na Mch. Filbert J. Mwanga

 

FUNGU KUU: YOELI 2:23, 28 – 30; YAKOBO 5:7,8; ZEKARIA 10:1.

UTANGULIZI

Somo la Roho Mtakatifu ni mojawapo ya masomo adimu sana kufundishwa ndani ya makanisa yetu. Pia ni somo ambalo ulimwengu umelipotosha vya kutosha kwani kila jambo watu wanalotenda wanadai wameongozwa na Roho ama amefunuliwa na Roho. Jambo hili limezidi kuwa la hatari zaidi kwani hata kipindi hiki wanaotoka na kuliacha kanisa wanadai Roho amewafunulia kuwa waondoke kanisani! Hivyo Roho Mtakatifu ametafsiriwa tofauti sana jinsi anavyotenda kazi katika maisha ya watu.

Roho Mtakatifu ana majina mengi katika Biblia. Ni somo pana linalohitaji umakini sana kulifundisha na hata kulielewa. Majina yake katika Biblia ameelezwa hivi: Roho wa Mungu, Ubatizo wa Moto, Ubatizo wa Roho, Mvua, Mvua ya Vuli, Mvua ya Masika, Mafuta, Kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana, Mfariji, Msaidizi, Roho wa Kweli, Muhuri wa Mungu; Mtakasaji, n.k. [Mathayo 3:11; Matendo 10:38; Yoeli 2:23; Efeso 1:13; n.k.]

Roho Mtakatifu ameelezewa kwa vipindi viwili tofauti ndani ya Biblia. Mvua ya Vuli na Mvua ya Masika. Biblia inapozungumzia mvua katika muktadha wa Roho haimaniishi kuwa Roho wa aina mbili, La! Bali ni tofauti mbili za utendaji wake kazi katika maisha ya mwanadamu hasa katika ukamilishaji kazi yake ya ukombozi maishani mwetu. Biblia inafundisha wazi kuwa mvua ya vuli ilimwagwa wakati ule wa Pentekoste; na mvua ya Masika itakapomwagwa mwishoni kabisha mwa kazi ya injili – yaani muda mfupi kabla ya mlango wa rehema kufungwa.

Hivyo tunapojifunza somo hili la Roho Mtakatifu tunapaswa kuelewa kuwa ni karama ya juu sana ambayo Kristo Yesu ametoa kwa kanisa lake baada tu ya kafara yake juu ya Msalaba wa Kalvari! Mama White anasema, “Katika kipawa cha Roho, Yesu alimpatia mwanadamu wema mkuu sana ambao mbingu ziliweza kutoa” (OHC 150)…. “Kabla ya Yeye mwenyewe kujitoa mhanga kuwa dhabihu yetu, Kristo alitafuta kipawa cha muhimu sana na kikamilifu ili kuwapatia wafuasi wake, kipawa ambacho kingeleta karibu sana nao nguvu za neema yake zisizokuwa na kikomo. Alisema ‘Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi Mwingine” (DA 668,669).

 

SOMO.

Wakristo wengi ulimwenguni wamechanganyikiwa na madai haya ya watu wanaotenda miujiza na unenaji bandia huku wakidai kuwa ni kipawa cha Roho Mtakatifu. Paulo alitoa tahadhari kubwa kuwa siku za mwisho zitakuwa nyakati za hatari watu wakisikiliza roho zidanganyazo na mafundisho ya Mashetani (1Timotheo 4:1). Zipo kanuni za msingi ambazo mkristo hupaswi kuchanganyikiwa unapohitaji kutambua Roho wa Kweli. Yesu alisema kanuni ya kwanza kutambua kuwa una Roho wa Kweli ni Kumpenda YESU kwa Kuzishika Amri zake zote kumi! (Yohana 14:15-17, 21, 23; Matendo 5:32). Hakuna Roho wa Kweli atakayetolewa kwa mtu awaye yote aliyeikanyaga sheria ya Mungu. Roho anakutia ndani ya ukweli wote! Huna haja ya kutazama miujiza au uponyaji au mahubiri ya kusisimua sana au huduma ya ukarimu kama ndicho kipimo cha watu wanaoongozwa na Roho wa Kweli! Tafuta matunda ya Roho Mtakatifu pekee yake ili kiwe ndicho kipimo cha ishara ya kuongozwa na Roho Mtakatifu. Soma Wagalatia 5:22, 23; Mathayo 7:19-20; Isaya 8:19-20.

Somo hili la Roho Mtakatifu limekuwa adimu sana ndani ya makanisa yetu, jambo ambalo limeleteleza huduma za maombi kupungua ndani ya makanisa yetu. Mama White anaeleza kuwa ilipasa tumfundishe Roho Mtakatifu kwa wingi kwani angeleta badiliko maishani mwetu. Anasema hivi: “… Yesu aliwatia moyo kwa kuwapa ahadi ya Roho Mtakatifu. Ahadi hiyo ni yetu sisi kama vile ilivyokuwa yao, lakini hata hivyo ni mara chache jinsi gani imewekwa mbele ya watu wetu, na kupokewa kwake kuongelewa kanisani. Kama matokeo ya ukimya huo juu ya somo hili muhimu sana, ni ahadi gani tunayojua habari zake kidogo kuhusu utimilizo wake halisi kuliko ahadi hii ya thamani ya kipawa cha Roho Mtakatifu, ambacho kupitia kwacho ufanisi wa kazi yetu yote ya kiroho unapatikana? Ahadi ya Roho Mtakatifu inatajwa katika hotuba zetu kwa nadra sana, yaani, inagusiwa kwa nasibu tu, na ndiyo yote. Unabii umehubiriwa sana, mafundisho ya Biblia yamefafanuliwa; lakini kile ambacho ni cha muhimu kwa kanisa ili lipate kukua katika nguvu za kiroho na ufanisi, ili mahubiri yaweze kuwa na nguvu ya usadikisho, na roho zipate kuongolewa kwa Mungu, kwa sehemu kubwa kimeachwa nje ya mahubiri ya wachungaji wetu.” (TM 174; 8T 21).

Ni kweli kabisa tumekuwa na hotuba kavu ambazo zimekosa mafuta ya Roho Mtakatifu. Lakini madai ya kuongozwa na Roho yameongezeka kwa wakristo ndani na nje ya kanisa. Kanisa inabidi lifundishwe kutambua matunda ya Roho katika maisha ya mkristo ili kuweze kupambanua roho wa uongo dhidi ya madai ya Roho wa kweli. Kanisa la siku za mwisho Yohana alilionya wazi wazi kuwa zitakuwa ni nyakati za hatari na udanganyifu mkuu. Yohana aliweka bayana kuwa usalama wetu utakuwa ni kuzipima hizo roho zinazodai kuwa Mungu amezungumza nazo. Unaposoma 1 Yohana 2:26 – 28; 4:1. Roho Mtakatifu ndiye ambaye ameachiwa dhamana ya kukamilisha kazi ya ukombozi wa mwanadamu (Efeso 1:13; 4:30). Tendo la kufuru ni pale tunapochukua hatua za kudharau sauti ya ushuhudiaji wa Roho Mtakatifu. Wengi wamefikiri kuwa Roho Mtakatifu sio nafsi kamili ya Uungu. Wengine wamepotoka na kudiriki kufundisha kuwa Roho Mtakatifu ni uwezo au nguvu ya Mungu katika utendaji kazi – hivyo kuna uwili Mtakatifu wala hakuna Utatu Mtakatifu. Hilo sio fundisho la kanisa wala Biblia bali ni la watu ambao wamechanganyikiwa katika kusoma Biblia. ROHO MTAKATIFU NI NAFSI KAMILI! Ni Mungu kamili! Ni nafsi ya TATU! NI SAWA NA BABA NA YESU – MWANA! Biblia imeeleza vizuri unaposoma MATENDO 5:3, 4; 1 YOHANA 5:7-9. Mama White anasema wazi kuwa, “Uovu ulikuwa ukilundikana kwa karne nyingi na ungeweza tu kuzuiwa na kupingwa kwa uweza mkuu wa Roho Mtakatifu, Nafsi ya Tatu ya Uungu, ambaye angekuja si katika nguvu iliyopunguzwa, bali katika utimilifu wa uweza wa Uungu” (TM 392).

Mvua ya vuli ilipomwagwa wakati wa Pentekoste dunia iliangazwa kwa Utukufu wake (Roho). Mama White anasema, “Kumwagwa kwa Roho katika siku zile za mitume ulikuwa ndio mwanzo wa mvua ya awali, au mvua ya vuli, na matokeo yake yalikuwa mazuri mno. Mpaka mwisho wa wakati Roho Mtakatifu atakaa ndani ya kanisa la Kweli” (AA 54, 55).

Yalikuwepo maandalizi ya msingi yaliyofanyika na mitume ili kupokea mvua ya vuli. Yapo mambo sita yaliyofanyika ili kupokea mvua ya vuli kwa mitume: 1. Waliomba kwa bidii. 2. Waliomba ili wafae kukutana na watu. Hawakukaa kivivu bila kazi. 3. Walijinyenyekeza mioyo yao kwa toba ya kweli na maungamo. 4. Waliweka mbali tofauti zao zote na tamaa yote ya madaraka. 5. Walimsogelea Mungu karibu zaidi kwa njia ya ibada – kusoma neno, kusifu, na kuomba. 6. Walikuwa na mzigo wa kuokoa roho za watu (Uinjilisti). Mama White anasema kuwa ili wapokee Roho walifanya hayo, “Hawakungoja kivivu. Kumbukumbu zinasema kwamba ‘walikuwa daima ndani ya hekalu, wakimsifu Mungu’ (Luka 24:53)… walijinyenyekeza mioyo yao kwa toba ya kweli na kuungama kutokuamini kwao…. Mitume waliomba kwa bidii sana ili waweze kufaa kukutana na watu na katika maongezi yao ya kila siku wapate kusema maneno yatakayowaleta wenye dhambi kwa Yesu…. Wakiweka mbali tofauti zao zote, na tamaa yote ya ukubwa, walishikamana pamoja katika ushirika wa Kikristo…. Ilikuwa ni baada ya wanafunzi kuwa na umoja kamili, walipokuwa hawashindanii tena vyeo, ndipo Roho alipomwagwa juu yao (8T 20)…. Walikuwa na mzigo wa wokovu wa roho za watu” (AA 35 – 37).

Mambo haya ndio yanayohitajika tuwe nayo kwa maandalizi ya kupokea mvua ya Masika. Hakuna yeyote atakayemwagiwa kipawa cha Roho wakati machungu na husuda kati ya mtu na mtu vinaendekezwa. Wakati kanisa litakapojishughulisha na kazi ya Baba wa Mbinguni mibaraka ya Roho ndiyo zawadi ya pekee itakayotolewa. Kugombaniana madaraka ndani ya kanisa ni kielelezo tosha kuwa hatuna Roho wa Kweli. Mama White anaendelea kusema kuwa Roho anapoingia maishani yapo mambo ya msingi yanayotendeka – uumbaji mpya- utu wa kale unatoweka – tunavaa kao jipya: “Chini ya utendaji wa Roho Mtakatifu, hata wale waliokuwa dhaifu kuliko wote, kwa kujizoeza imani yao kwa Mungu, walijifunza kukuza uwezo waliokabidhiwa na kutakaswa, kusafishwa, na kuwa waungwana. Kadiri walivyojiweka chini ya mvuto wa kuumba wa Roho Mtakatifu, walipokea utimilifu wote wa Uungu, nao waliumbika kwa sura yake Mungu” (AA 49, 50).

Mvua ya masika inamwagwa tu mahali ambapo chombo chote kimesafishwa mbali na taka zote za dhambi. Wakati magomvi yamekoma kanisani, wivu, kijicho, malumbano, na hata uzembe katika kazi ya Mungu umetoweka. Mvua ya masika inamwagwa mara kumi zaidi ya mvua ya vuli. Mvua ya masika inatolewa kwa kusudi ya kuliandaa kanisa au mkristo kusimama katika jaribu kuu la mwisho – jumapili. Ni wale wote tu ambao wamepokea mvua ya vuli watakaopokea mvua ya masika (kugongwa muhuri wa Mungu). Kama vuli haikufanya kazi maishani mwangu basi nchi haiwezi kuvunwa. Mavuno ya nchi yanakamilika pale tu yanapopokea mvua ya kwanza na ya mwisho (Vuli na Masika). Wengi wanafikiri vuli ilikoma wakati wa mitume, la! Mvua ya vuli inakwenda mpaka mwisho wa wakati – mlango wa rehema utakapofungwa. Swali kwanini makanisa yetu hayana uamsho wa mvua ya vuli. Jawabu Mama White anasema, “Bwana hakufunga hazina ya mbinguni baada ya kuwamwagia Roho wake wanafunzi wale wa awali. …. Kama sisi hatuna nguvu zake, ni kwa sababu ya ulegevu wa kiroho, hali yetu ya kutojali, na uvivu. Hebu na tuondokane na hali hiyo ya kufuata desturi na kuwa kama wafu” (6BC 1055).

Nitawezaje kumpata Roho wa Kweli maishani mwangu? Nitawezaje kumdumisha Roho wa Mungu asitoweke maishani mwangu? Biblia na Roho ya Unabii inaweka bayana kuwa ni kwa njia ya maombi ya dhati na kufanya kazi ya Mungu kwa bidii (Luka 11:13). Mama White anasema, “Inawezekana tumekuwa na kiasi Fulani cha Roho wa Mungu, lakini kwa njia ya maombi na imani tunapaswa kutafuta daima kujazwa zaidi na Roho. Haitafaa kitu kabisa kuacha juhudi zetu. Tusiposonga mbele, kama hatujiweki wenyewe katika msimamo wa kuweza kupokea mvua ya awali na mvua ya masika, basi, tutapoteza roho zetu, na uwajibikaji utakuwa mlangoni petu.” (TM 508). … Kipimo cha Roho Mtakatifu tuanachopokea kitalingana na kiwango cha shauku tuliyo nayo na imani itumikayo ili kukipata, na jinsi tutakavyotumia nuru na maarifa tutakayopewa. Tutaaminiwa kipawa cha Roho Mtakatifu kulingana na uwezo wetu wa kupokea na kugawa kwa wengine” (RH 5/5/1896).

MWITO

Kama kazi ya injili ilivyoanza kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, ndivyo itakavyofungwa kwa udhihirisho mkuu wa Roho huyo huyo! Maajabu makuu yataonekana dhahiri jambo ambalo litawachanganya wengi – waovu watafanya miujiza na pia watu wa Mungu kadhalika. Mama White anasema kuwa, “Kazi kuu ya injili haitafungwa kwa udhihirisho kidogo wa uweza wa Mungu kuliko ule ulioashiria mwanzo wake. Unabii uliotimizwa katika kumwagwa kwa mvua ya vuli mwanzoni mwa kazi ya injili utatimizwa tena katika mvua ya masika wakati wa kufungwa kwake. Hapa ndipo zilipo zile ‘nyakati za kuburudishwa’ ambazo mtume Petro alikuwa akizitazamia kuja aliposema: ‘Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate kumtuma Kristo Yesu’ (Matendo 3:19, 20). … kazi hiyo itafanana na ile iliyofanyika siku ya Pentekoste” (GC 611, 612).

Wengi wanangojea kwa kutazama ubichi wa kazi ya injili katika mabara na mahali mbalimbali kuwa bado sana. Huu ndio udanganyifu mkuu wa Shetani ambao atawafanya wengi washindwe kupokea mvua ya masika wakingojea kuona badiliko Fulani ndani ya kanisa. Uamsho wa kweli ni watu mmoja mmoja peke yake. Mama white anasema kuwa: “Je, tunatarajia kuona kanisa lote likiwa limeamka? Wakati huo hautakuja kamwe. Kuna watu ndani ya kanisa ambao hawajaongoka, na ambao hawatajiunga katika maombi ya dhati na ya kudumu. Imetupasa kuingia katika kazi hiyo kila mtu peke yake. Yatupasa kuomba sana, na kuzungumza kidogo” (1SM 122). … Wale wasiofanya juhudi yoyote ya dhati, bali wanangojea tu Roho Mtakatifu awalazimishe kutenda kazi, wataangamia gizani. Haiwapasi kukaa kimya bila kufanya chochote katika kazi ya Mungu.” (ChS 228).

Tumwombe Bwana wa Mavuno atupatia haki yake upesi! Kipawa cha Roho Mtakatifu!

 

 

SOMO LA SABA.

MUHURI WA MUNGU AU ALAMA YA MNYAMA.

Imeandaliwa na Mch. Filbert J. Mwanga

 

FUNGU KUU: UFUNUO 7:1-4; 13:14-18; 14:9 – 11; 16:2; EZEKIELI 9:1 - 6.

UTANGULIZI

Ulimwengu unakwenda kufikia mwisho wake. Kama ulivyoanza kwa kambi mbili baada ya dhambi kuingia- alama ya Kaini na Damu ya Habili! Ndivyo itakavyofungwa kwa kambi mbili tena. Kambi ya Kristo na Shetani – Muhuri wa Mungu au Alama ya Mnyama. Makundi haya mawili yapo kila dhehebu au dini yeyote duniani. Makundi haya yatakwenda sambasamba mpaka mwisho wa wakati. Muda mfupi kabla ya mlango wa rehema kufungwa kila mwanadamu atakayekuwa hai atakuwa amechagua upande wa kusimama. Kupokea alama ya mnyama ama kupokea muhuri wa Mungu. Kipimo cha mwisho na jaribu kuu la mwisho limejengwa katika UTII kama ilivyokuwa pale Edeni. Matunda yote Adamu alipewa kuyatunza na kuyatumia kasoro mti mmoja wa ujuzi wa mema na mabaya. Haukuwa na utamu au sumu tofauti na miti mingine, bali ulikuwa na tamko la Mungu kwamba USILE! Ulikuwa ni kipimo cha utii! Mungu ameweka siku saba katika juma. Siku zote zipo sawa machoni pa wanadamu wote. Bali kuna siku moja tu ambayo Mungu amesema TUSIITUMIE kwa shughuli zetu! Nayo ni siku ya Saba. Kutoka 31:12 – 17; 20:8-11. Hii ni amri ya milele. Lakini watu wamefanya mchezo ule ule wa Adamu na Hawa. Wameitumia kwa shughuli zao za maisha.

Nyakati zinakuja siku ya Saba itasimama kama kipimo cha utii kwa wanadamu wote. Uamuzi usioyumba utaamuliwa juu ya maisha ya watu kwa namna tutakavyojibu kuhusiana na amri hii ya nne. Wengi wetu ndani ya kanisa tunaisogelea Sabato kama Hawa kwa kuiona kuwa ni siku ya kutamanika kwa kununua vocha zetu, kupasi, kutazama Televesheni, kupasi nguo, kununua vitu au kuuza kwa njia ya simu, usomaji wa magazeti siku ya Sabato ama kuangalia mipira na michezo ya kuigiza siku ya Sabato. Matendo hayo yote yanatupelekea katika uasi na uhalifu wa amri hii ya Mungu kwa kuiona siku hii kuwa sawa na nyingine. Jumapili na Jumamosi ndiyo kipimo pekee kitakachoamua kupokea alama ya mnyama au muhuri wa Mungu. Mama White anasema kuwa: “Ishara au muhuri wa Mungu umefunuliwa katika utunzaji wa Sabato ya siku ya Saba, ukumbusho wa Bwana wa uumbaji… Chapa ya mnyama ni kinyume cha hii – utunzaji wa siku ya kwanza ya juma.” – 8T 117 (1904).

 

SOMO

MUHURI WA MUNGU

Muhuri wa Mungu unatiwa katika vipaji vya uso na wala sio katika mikono (Ufunuo 7:3; 14:1). Muhuri wa Mungu unatiwa katika paji la uso ikimaanisha lazima kila moja aukubali wokovu kwa hiari yake na sio kwa kulazimishwa. Muhuri wa Mungu ni tabia ya Kristo maishani mwetu. Ni alama ya Roho Mtakatifu maishani mwetu (Efeso 1:13). Mama White anasema kuwa: “Si muhuri au alama inayoweza kuonekana kwa macho, bali ni kule kutulia katika kweli, kiakili na kiroho, hata wasiweze kuondoshwa – mara tu watu wa Mungu watakapokuwa wametiwa muhuri na kutayarishwa kwa ajili ya kupepetwa, basi, kutakuja” (4BC 1161). Unapotunza amri kumi za Mungu chini ya maongozi ya Yesu Kristo maana yake ni kuivaa tabia Kristo. Mama White anasema kuwa, “Muhuri wa Mungu aliye hai utawekwa tu juu ya wale wanaofanana na Kristo kitabia” (7BC 970).

Katika amri kumi za Mungu ipo alama moja tu ya kuwatambua wale ambao walio na muhuri wa Mungu. Ni Sabato ya Siku ya Saba ya Juma. Utunzaji wa Sabato unaozungumzwa hapa sio utunzaji wa dini bali mahusiano yetu na Mungu tunayokuwa nayo katika ibada yake takatifu. Wapo wengi ambao wanaoitwa Wasabato lakini haiamanishi kuwa watakuwa na muhuri wa Mungu. Zingatia muhuri wa Mungu ni tabia ya Yesu maishani mwetu. Kumvaa Bwana Yesu kikamilifu! Mama White anaeleza swala la Sabato kama muhuri wa Mungu wakati wa pambano kuu la mwisho katika jumapili na Sabato ya Kweli – Jumamosi. Anasema kuwa, “Utunzaji sahihi wa Sabato ndiyo ishara ya utii wetu kwa Mungu” (7BC 981).

Sabato ya siku ya Sabato itakuwa ni ishara ya kuwatambua watu wa Mungu pale tu watakapojitoa kuitunza kwa usahihi na pia kusimama imara wakati wa jaribu kuu la mwisho. Paulo anasema kuwa “Imesalia raha ya Sabato kwa watu wa Mungu” – Waebrania 4:9-11. Anakazia kwa kusema kuwa raha hiyo tunaingia kwa kupumzika kama Mungu alivyopumzika na kuacha kufanya zetu siku ya Sabato. Hivyo muhuri wa Mungu aliye hai kwa watu wa Mungu wa siku za mwisho ni SABATO! Mama White anasema,

“Kutakuwa na alama itakayowekwa juu ya watu wa Mungu, na alama hiyo ni utunzaji wa Sabato yake takatifu” (7BC 981)…. Kwetu, Sabato imetolewa kuwa ‘agano la milele’ sawa na ilivyokuwa katika Israeli. Kwa wale wanaoiheshimu sana siku yake takatifu, Sabato ni ishara inayoonyesha kwamba Mungu anawatambua wao kuwa ndio watu wake wateule. Ni ahadi yake kwamba atawatimizia agano lake. Kila roho inayopokea ishara ya serikali ya Mungu inajiweka yenyewe chini ya agano lake takatifu na la milele. Inajifungamanisha yenyewe kwenye mnyororo wa dhahabu wa utii, ambao kila pete yake ni ahadi. Ni amri ya nne peke yake katika zile kumi iliyo na muhuri wa Mtoa-Sheria Mkuu, Muumba wa mbingu na nchi” (6T 350; PP 307).

Wale wote watakaopokea muhuri wa Mungu na kukubaliwa kuuridhi uzima wa milele wanapaswa kuwa na sifa zifuatazo:

  1. Watakuwa ni watu walioangazwa na Neno la Mungu.  “Umwagaji mkuu wa Roho wa Mungu ambao unaangaza dunia kwa utukufu wake, hautakuja mpaka tuwe watu walioangazwa”. – Review and Herald, May 29, 1826.
  2. Wamekuwa washindi wa dhambi maishani mwao. Ushindi usiokoma wa dhambi.
  3. Watakuwa watu wenye upendo – upendo wa kidugu – wenye shauku kuona wengine wanaokolewa. “Kila alichosema Yesu pendaneni ninyi kwa ninyi kitakapotiliwa maanani ndani ya waumini-wivu, chuki, masengenyo, mawazo mabaya hayatatamanika tena: hayatakuwa na sehemu katika ujenzi wa tabia.” – Review and Herald, October 6, 1890. 
  4. Watu wenye maombi ya dhati na tena binafsi. “Lakini Mungu ni lazima aamuru mvua kunyesha. Hivyo hatupaswi kuzembea maombi na dua…Hebu tukiwa pamoja na mioyo iliyotubu, tuombe sana kwa dhati kwamba sasa, wakati wa mvua ya masika, manyunyu ya neema yaweze kutumwagia juu yetu”. – Testimonies to Ministers, p. 590. 
  5. Watu wanaofanya kazi ya Mungu – kuokoa roho za watu. “Umwagwaji mkuu wa Roho Mtakatifu, ambao uliangaza dunia yote kwa utukufu wake, hautakuja mpaka tuwe watu walioangazwa, kwamba kujua kwa uzoefu inamaanisha nini kuwa watendakazi pamoja na Mungu. Wakati tutakapojitoa moyo wote wakfu kwa kazi ya huduma ya Kristo, Mungu atautambua ukweli huu kwa kumwagwa kwa Roho wake pasipo kipimo; lakini hili halitakuwa wakati sehemu kubwa ya kanisa siyo watendakazi pamoja na Mungu” – Christian Service uk. 253 (EV. 699). Kazi ya umishonari inaamsha roho na kuleta kwa wingi zaidi Roho Mtakatifu katika maisha ya mkristo. Maana ni kweli kuwa “kanuni ya kujihudumia mwenyewe ni kanuni ya kujiangamiza mwenyewe. Kanuni ya kujitoa mwenyewe ni kanuni ya kujihifadhi (kujitunza) mwenyewe”. DA, uk. 623.  
  6. Watu wenye kiasi. Wanaoishi kwa kanuni za afya ya kimwili, kiroho na kiakili. “kuwa na kiasi hutufundisha kutokutumia kabisa kitu chochote chenye kudhuru na kutumia kwa busara vile vitiavyo afya”.-Patriach and Prophets, uk. 562 [1890]. “uvunjaji wa kanuni za mwili ni uvunjaji wa kanuni za Mungu … kila tendo ambalo linaharibu mwili, akili na uwezo wa kiroho ni dhambi”. – CDF, p. 43. 
  7. Wanaoutunza Sabato kikamilifu na Amri zote Kumi za Mungu Isaya 56:1-2.

 

ALAMA YA MNYAMA

Alama ya mnyama ni kitambulisho cha wale wote waliokataa neema ya Kristo. Wamekataa huruma za Mungu katika maisha yao. Alama ya mnyama ni kinyume cha Muhuri wa Mungu. Alama ya mnyama inatiwa katika paji la uso na katika mkono wa kuume. Hili linaamanisha kuwa wale watakaopokea kwenye paji la uso ni wale waliofanya uchaguzi wao binafsi wa kutomkutii Mungu. Katika mkono wa kuume ni wale ambao wamelazimika kupokea kwa sababu ya hali ya uchumi au ulazimishwaji kwa njia ya mateso. Mama White anasema kuwa: “Chapa ya mnyama ni sabato ya kipapa. (EV 234)…. Wakati wa kupimwa utakapofika, itaonyeshwa dhahiri kile ilicho chapa ya mnyama. Ni utunzaji wa Jumapili” (7BC 980).

Je kuna watu ambao wamepokea alama ya mnyama sasa? Jawabu la! Jumapili itakuwa alama ya mnyama mara itakapowekwa kama sheria ya siku ya kuabudu kinyume cha Sabato ya siku ya Saba – Jumamosi! Mama White anasema kuwa: “Utunzaji wa Jumapili bado siyo chapa ya mnyama, na haitakuwa mpaka amri kuu imetolewa ikiwafanya watu kuiabudu sanamu hii ya Sabato. Wakati utafika ambapo siku hii itakuwa ndicho kipimo, lakini wakati huo bado haujafika” (7BC 977; Matukio, uk. 205, 206). “Hakuna mtu yeyote mpaka sasa aliyekwisha kupokea alama ya mnyama” (Ev 234).

Ni wakati gani alama ya mnyama itakuwa imepokelewa maishani mwa mtu? Ni pale atakapokuwa amepata ukweli wote juu ya Sabato ya Kweli, kisha akaendelea kukataa hata mara baada ya sheria ya kuabudu siku ya Jumapili itakapokuwa imetangazwa. Mama White anasema, “Wakati utunzaji wa Jumapili utakaposhurutishwa kwa sheria, na ulimwengu utakapokuwa umepata nuru juu ya uwajibikaji wa kutunza Sabato ya kweli, hapo yeyote Yule atakayeasi amri ya Mungu ili aitii kanuni ambayo haina mamlaka ya juu zaidi ya yale ya Roma, atakuwa hivyo anaheshimu upapa zaidi ya Mungu. Anatoa heshima kwa Roma, na kwa mamlaka yanayoshurutisha taasisi iliyoagizwa na Roma. Anaabudu mnyama na sanamu yake.” Matukio, uk. 206, 207.

 

MWITO.

Maandalizi ya kupokea muhuri wa Mungu ni tendo ambalo lisilo la bahati nasibu. Maandalizi ya msingi yanachukua maisha mkristo ya kuwa na uzoefu na Mungu wakati wote wa maisha yake. Mungu anatoa wito wake kwetu kuwa kila mmoja wetu azikabidhi njia zake mbele za Bwana ili atuongoze hatua zetu za maisha yetu. Na hatimaye kukimbia ajali kuu inayoujilia ulimwengu wote. Mama White anazungumzia kipindi hiki cha amani tulicho nacho ndicho cha kufanya maandalizi yote ya msingi ya kuachana na dhambi na kudumu katika kweli kwa kusema kuwa: “Kama waumini katika ukweli hawakutegemezwa na imani yao angalau katika siku hizi za amani, ni nini kitakacho waimarisha wakati kipimo kikubwa kitakapokuja na amri kutolewa dhidi ya wale wote ambao hawataabudu sanamu ya mnyama na kupokea chapa yake katika vipaji vya nyuso zao au katika mikono yao? Kipindi hiki kizito hakiko mbali sana. Baada ya kuwa wadhaifu na kutokuwa dhabiti, watu wa Mungu wangepaswa kuwa wanakusanya nguvu na ujasiri kwa ajili ya wakati wa taabu. – 4T 251 (1876). Matukio, uk. 204.

“Katika pambano kuu kati ya imani na kutoamini ulimwengu mzima Kikristo utahusika. Wote watachagua upande wa kusimama. Wengine yawezekana hawajishughulishi na upande wowote katika pambano. Waweza wasionekane wakichagua upande kinyume cha ukweli, lakini pia hawatajitokeza kwa ujasiri kwa ajili ya Kristo kwa sababu ya hofu ya kupoteza mali au ya kupatwa na shutuma. Wote hawa wanahesabiwa pamoja na maadui wa Kristo.” RH Feb. 7, 1893.

Lazima kila mtu achukue msimamo dhabiti dhidi ya kweli za Mungu: kutii ukweli au kuasi. Mama White anasema tusilee dhambi: “Ngome ya uovu iliyo imara zaidi ya zote katika ulimwengu wetu siyo mdhambi kuishi maisha ya uovu wa kupindukia au maisha ya kujivunjia heshima na kutengwa na jamii bali ni maisha yale ambayo vinginevyo yaonekana kuwa yenye uadilifu, ya heshima ya adili lakini ambayo ndani yake dhambi MOJA inalelewa, uovu MMOJA unaendekezwa …. Kipaji kikubwa na uelekevu, talanta, huruma, ukarimu na matendo ya wema, hivi vyote vyaweza kutumia kama mtego wa Shetani kuwashawishi watu waje kwenye poromoko la uangamivu.” – (Ed. 150; Matukio, uk. 143, 144.) WITO: Tuache kulea na kunyonyesha dhambi yeyote ndani ya kanisa ama familia zetu ili tuweze kupokea mvua ya masika!

 

VITABU VILIVYOTUMIKA KUANDAA MASOMO HAYA NI:-

  1. DHIKI KUU INAKUJA LAKINI KUNA TUMAINI: Sura 1 – 15.
  2. MATUKIO YA SIKU ZA MWISHO (Toleo la kwanza: Sura 11, 12, 13,15.)

VIFUPISHO VYA VITABU VILIVYOTUMIKA

1. AA – The Acts of the Apostles

2. BC – The Seventh-day Adentist Bible Commentary (with Ellen White Comments).

3. CDF – Counsels on Diet and Food

4. CM – Colpoteur Ministry

5. Ed – Education.

6. EV – Evangelism

7. GC – Great Controversy Between Christ and Satan

8. OHC – Our High Calling.

9. T – Testimonies for the Church

10. EW – Early Writtings.

11. FE – Fundamentals of Christian Education.

12. ChS – Christian Service

13. PK - Prophets and Kings

14. PP – Patriachs and Prophets

15. TM – Testimonies to Ministers

16. RH – Review and Herald

17. SM – Selected Messages

18. SP – The Spirit of Prophecy

SOMO HILI: LITATUMIKA MAKANISANI NA MAKUNDINI KWA AJILI YA JUMA HILI MAALUMU LA MAOMBI. SABATO YA MWISHO ITAKUWA NI SIKU YA KUFUNGA NA KUOMBA! BWANA AWATANGULIE KATIKA HUDUMA ZOTE NA HUSUSANI MAANDALIZI YA UMWAGWAJI WA MVUA YA MASIKA!

 

Who's Online

We have 4 guests online

Sikiliza Morning Star Radio

CALENDAR

Content on this page requires a newer version of Adobe Flash Player.

Get Adobe Flash player

BIBLE