Uamsho na Matengenezo 1

 

 

SOUTHERN HIGHLANDS CONFERENCE

 

 

 

 

 

 

JUMA LA MAOMBI 2012: UAMSHO NA MATENGENEZO!!!

 

JANUARI 4 – 14, 2012 SIKU 10 ZA MAOMBI!

 

 

GC: UAMSHO KWA UTUME.

 

ECD: ULIOKUSUDIWA KWENDA KWA KASI

 

TUM: KWA KUWEZESHWA NA ROHO MTAKATIFU.

 

 

GC + ECD +TUM: UAMSHO KWA UTUME ULIOKUSUDIWA KWENDA KWA KASI

KWA KUWEZESHWA NA ROHO MTAKATIFU.

 

 

 

“Uamsho na matengenezo lazima yafanyike , chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu. Uamsho na matengenezo ni vitu viwili tofauti. Uamsho humaanisha kufanyizwa upya kwa maisha ya kiroho, uamshaji wa nguvu za akili na moyo, ufufuo kutoka kwa kifo cha kiroho. Matengenezo humaanisha kugeuza taratibu, badiliko katika maoni na nadharia, tabia na matendo. Matengenezo hayataleta tunda zuri la haki isipokuwa tu yameshikamanishwa na uamsho wa Roho. Uamsho na Matengenezo havina budi kufanya kazi yake, na katika kuifanya kazi hii lazima vifanye kwa pamoja.” – MATUKIO YA SIKU ZA MWISHO, UK. 131.

 

 

WITO WA HARAKA: ‘KILA MUUMINI, MSHIRIKI, TAWI, KUNDI, KANISA, TAASISI NA ULIMWENGU MZIMA TUFANYE MATENGENEZO KATIKA UTENDAJI WETU, KUISHI KWETU, NA KULA NA KUNYWA KWETU ILI TUPATE KUPOKEA MVUA YA MASIKA.’

 

 

SOMO HILI IMEANDALIWA KWA AJILI YA JUMA LA MAOMBI YA MWAKA 2012

 

 

IMEANDALIWA NA IDARA YA HUDUMA ZA KICHUNGAJI NA WASHIRIKI

Mch. Filbert Joseph Mwanga

Mkuu wa Huduma za Washiriki – SHC.

 

 

 

SOMO LA KWANZA.

DHIKI KUU INAKUJA LAKINI KUNA TUMAINI LA UZIMA!

Imeandaliwa na Mch. Filbert J. Mwanga

 

FUNGU KUU: DANIELI 12:1

UTANGULIZI

Jambo lolote linapozungumzwa ndani ya Biblia lazima litatimia kwa wakati wake. Linaweza likawa ni jambo lisiloweza kuelezeka vyema kwa lugha za wanadamu lakini bado likawa na picha isiyofahamika vyema likabakia jambo la kuogofya unapolisoma ama kulisikia linapoelezewa. Danieli anafunga ujumbe wake kwa kuanza na kauli ambayo inatoa majumuisho ya pambano kuu kati ya wema na uovu. Kisha dunia kubaki na makundi mawili ya watu.

Mama White anapoyaangalia matukio ya mwisho na kufunga historia ya dunia hii anatoa tamko hili, “Dhiki kuu ya kutisha. Kazi ambayo kanisa limeshindwa kufanya katika kipindi cha amani na usitawi, litapaswa kuifanya katika kipindi cha dhiki kuu ya kutisha, katika mazingira ya kukatisha tamaa na kuogofya sana” (5T463; Ev. 31).

Mungu hakutuacha tu ili tuvamiwe na dhiki hiyo bila maandalizi ya kutosha. Hakika Mungu ni mwema kwa nyakati zote ameweka dalili za nyakati ili wote wapate kuokolewa ikiwa tu tutazingatia ishara hizo katika njia yote. Ametupatia kitu ambacho ni mwongozo wa njia (Roadmap towards heaven). Mama White anasema kuwa:

“Matukio ya yanayohusiana na kufungwa kwa mlango wa rehema na kazi ya matayarisho kwa ajili ya wakati wa taabu, vimeelezewa kwa wazi. Lakini makutano ya watu hawana ufahamu wowote zaidi wa kweli hizi muhimu sawa na kama kweli hizo zisingekuwa zimefunuliwa kwao kamwe …Amepewa ramani inayoonyesha kila alama ya njiani katika safari yake kuelekea mbinguni, wala hawapaswi kukisia kitu cho chote” (GC 594, 598).

 

  Mambo makuu ambayo Mungu ameyaweka bayana “Majanga katika nchi kavu na baharini, hali ya vurugu katika jamii, tahadhari za vita, ni ya kutisha. Yanabashiri juu ya matukio makuu yanayokaribia.”(9T 11). Swali kubwa je tumejiandaa katika pambano kuu la mwisho kusimama kwa miguu yetu mwenyewe bila kutegemea wazazi, wachungaji, ama waumini wenzetu. Ni dhoruba, “Dhoruba inaanza ambayo itaujaribu na kuutikisa kwa ghafla msingi wa kiroho wa kila mmoja wetu kwa upeo wa juu sana” (5T 129).

Somo hili nyeti sana kwa kanisa hili la siku za mwisho. Washiriki wetu wanapaswa kuwa walimu wa kuyajua maandiko na pia kuzijua dalili za nyakati. Hebu viongozi wa kanisa watumie muda wao vizuri katika kuwakilisha somo akilini mwa watu watambue nyakati tunazoishi sio za malumbano, utendaji wa uovu, ama kuishi maisha ya uzembe. Mama White anasema kuwa,

“Jitihada kubwa hazina budi kufanyika ili kuliweka somo hili mbele za watu. Ukweli huu wa kutisha unapaswa kuwekwa sio tu mbele ya watu wa ulimwengu, bali pia mbele ya makanisa yetu, kwamba siku ya Bwana itakuja ghafula, bila kutazamia. Onyo la kutisha la unabii huu linaelekezwa kwa kila roho. Hebu asiwepo hata mmoja anayejisikia kuwa yu salama mbali na hatari ya kushtukizwa. Hebu tafsiri ya mtu mwingine awaye yote ya unabii isikunyang’anye usadikisho wa kuyajua matukio ambayo yanaonyesha kuwa tukio hilo kuu limekaribia sana” (FE 336).

 

SOMO

Yapo matukio ambayo yametabiriwa katika Maandiko Matakatifu na Roho ya Unabii yanachukua hatua zake machoni petu leo. Unaposoma LUKA 21:25 – 36 Yesu alitabiri mambo ya siku za Mwisho kuwa kabla ya dhiki hiyo inayokuja dunia itafikwa na maafa makubwa yatachanganya wakuu wa dunia hii kuhimili dhoruba zake. Mama Ellen G. White anasema,

“Tunasimama kwenye kilele cha dhiki kuu ya zama zote. Kwa mfuatano wa haraka haraka hukumu za Mungu zitakuja moja baada ya nyingine – moto, na mafuriko, na matetemeko ya nchi, pamoja na vita na umwagaji damu. Hatupaswi kushangazwa wakati huu na matukio haya makuu na ya kukata maneno; kwani malaika wa rehema hawezi kuendelea kwa muda mrefu zaidi kuwakinga wale wasiotubu” (PK 278). …“Wakati wa sasa ni wakati wa kusisimua mno kwa wote wenye uhai. Watawala na viongozi wa siasa, watu wanaoshika nafasi zenye dhamana na mamlaka, wanaume na wanawake wenye kufikiri sana wa tabaka zote, wamekaza mawazo yao juu ya matukio yanayotokea kutuzunguka. Wanafuatilia mahusiano yaliyopo miongoni mwa mataifa. Wanachunguza nguvu inayotwaa udhibiti wa kila kitu cha asili, na wanatambua kuwa jambo Fulani kubwa na la kukata maneno li karibu kutokea, - kwamba ulimwengu upo ukingoni mwa dhiki kubwa sana” (PK 537; Ev. 703, 704; Ed. 179).

Muungano wa Makanisa:

Tunapoangalia viongozi wa ulimwengu hakika wamechanganyikiwa katika matukio yanayosibu ulimwengu wetu, itafika wakati watahitaji msaada wa viongozi wa kidini. Kumbe upande wa pili wa viongozi wa kidini nao watahitaji kuungana mikono katika uasi wa Amri za Mungu kwa kufanya maridhiano ya mafundisho yao. Hatimaye ndipo viongozi hawa wa dini watakapotoa mkono kwa watawala wa dunia hii. Mama White anaeleza hatua hizi kuwa,“Wakati makanisa makuu ya Marekani, yatakapoungana katika yale mafundisho wanayoyashikilia kwa pamoja, yataishawishi serikali kuyatia nguvu kisheria maagizo yao na kuzitegemeza desturi zao, ndipo Marekani ya Kiprotenstanti itakuwa imeunda sanamu ya utawala wa kidini wa Rumi, na ndipo utoaji adhabu ya kiserikali kwa wale wanaopinga utakuwa jambo lisiloepukika” (GC 445).

Muungano wa Kanisa na Serikali:

Kitabu cha Ufunuo 17:3 kinataja muungano wa kanisa la Serikali. Tunapochunguza Biblia hakuna fungu linaashiria kuwa kutakuwepo na muungano wa serikali na serikali kama inavyoonekana leo katika vikao vya dunia. Mambo hayo yote yataishia kwenye karatasi za vikao tu. Lakini Biblia inatuonyesha mamlaka za dunia zitauungana na Kanisa asi kwa kupeana mkono na upapa. Mama White anaeleza bayana:

“Waprotestanti … wanafungua mlango kwa upapa kupata tena katika Marekani ya Kiprotestanti mamlaka ambayo uliyoyapoteza katika Ulimwengu wa Zamani…Waprotestanti wa Marekani watakuwa mstari wa mbele katika kunyosha mikono yao juu ya shimo kubwa na kuushika mkono Umizimu; watanyosha mikono juu ya shimo kubwa na kushikana mikono na Mamlaka ya Rumi; na chini ya uongozi wa muungano huo wa utatu [Uprotestanti, Umizimu, na Ukatoliki], nchi hii itafuata katika nyayo za Rumi kwa kukandamiza uhuru wa dhamiri” (GC 573, 588)….“Wakati Uprotestanti utakaponyosha mkono kuvuka shimo kubwa na kuushika mkono wa Mamlaka ya Rumi, wakati utakaponyosha mkono juu ya shimo kubwa na kushikana mikono ya Umizimu, wakati chini ya uongozi wa muungano huo wa utatu, nchi yetu [Marekani] itakapokuwa imeikataa kila kanuni ya Katiba yake kama Serikali ya Kiprotestanti na ya Jamhuri, na kuandaa njia kwa ajili ya kueneza uongo na udanganyifu wa upapa, ndipo tunaweza kujua kwamba wakati umewadia kwa utendaji wa miujiza wa ajabu wa Shetani na kwamba mwisho u karibu” (5T 451).

Taasisi zetu za elimu zinapaswa ziwe na waalimu ambao wanaujumbe wa onyo la mwisho akilini mwao na pia wawafunulia wanafunzi wetu habari hii ili waweze kuandaliwa kwa pambano kuu la mwisho – kati ya wema na uovu. Mama White anasema, “Katika majira ya usiku maneno haya yalinenwa kwangu: Waagize walimu katika shule zetu kuwatayarisha wanafunzi wao kwa kile kinachoujia ulimwengu” (FE 526, 527).

 Muungano huu wa makanisa na serikali za kidunia utaondoa uhuru wa dhamira wa kuabudu kwa kukataza mahubiri ya hadhara ama utangazaji wa injili kwa njia mbalimbali. Lakini wakati huo ndipo wainjilisti, Madaktari na waumini watakapopata fursa ya kusambaza ujumbe wetu kwa njia ya vitabu, magazeti, na vijizuu kwa kupeleka nyumba kwa nyumba. Mama White anasema kuwa “Maadamu muda wa majaribio bado ungalipo, kutakuwepo na nafasi kwa mwinjilisti wa vitabu kufanya kazi. Wakati madhehebu za dini zitakapoungana na upapa ili kuwatesa watu wa Mungu, mahali palipo na uhuru wa dini patafunguliwa kwa uinjilisti wa vitabu” (6T 478).

Mama White anasema kuwa: “Jumapili yaweza kutumiwa kuendesha kazi mbalimbali ambazo zitatimiza mambo mengi kwa ajili ya Bwana. Katika siku hii mikutano ya nje na ndani yaweza kufanyika. Kazi ya nyumba nyumba yaweza kufanyika. Wale ambao ni waandishi watumie muda huu kuandika nakala zao. Kunapowezekana mikutano ya dini ifanyike jumapili. Fanyeni mikutano hii iwe ya kuvutia sana. Imbeni nyimbo nzuri za uamsho, na hubiri kwa nguvu juu ya Mwokozi wa Upendo na ahadi zake za hakika… Wachukueni wanafunzi nje wakafanye mikutano katika sehemu mbalimbali, na kufanya kazi ya umishonari kwa njia ya uganga. Watakutana na watu katika majumba yao, na hapo watapata nafasi nzuri kuwapatia ukweli. Kutumia siku ya jumapili kwa njia hii ni jambo linalokubalika mbele za Bwana.” (9T 238).

 

MWITO

Usalama wetu pekee dhidi ya udanganyaji mkuu wa kuogofya katika dunia sio katika maneno ya kujifariji na matumaini pekee bali ni katika kuweka mizizi yetu katika ukweli wa Neno la Mungu. Wapo wengi ambao wamekuwa na faraja za vyeo ndani ya kanisa, mahudhurio ya ibada, na hata kufanya matendo mema kwa jamii; lakini tumesahau kuwa usalama wetu pekee ni kuweka nang’a yetu miguuni pa Yesu Kristo. Mama White anasema kuwa,

“Ni wale tu walioimarisha akili zao kwa kweli za Biblia ndio watakaoweza kusimama imara katika pambano kuu la Mwisho (GC 593)… Jifunze Biblia yako kwa namna ambayo hujawahi kamwe kujifunza siku za nyuma. Isipokuwa unainuka na kufikia kiwango cha juu cha utakatifu katika maisha yako ya dini, hutakuwa tayari kwa ajili ya kufunuliwa kwa Bwana wetu” (5T717)…“Ni wale tu ambao wamekuwa wanafunzi wenye bidii wa Maandiko, na ambao wameipenda hiyo kweli, watakaolindwa dhidi ya madanganyo yenye nguvu yatakayouteka ulimwengu wote (GC 625)… “Tunazikaribia nyakati za dhoruba … kila msimamo wa imani yetu utachunguzwa; na ikiwa sisi si wanafunzi kamili wa Biblia, tuliothibitika, tulioimarishwa, na kutulia katika kweli, basi, hekima ya watu mashuhuri wa ulimwengu huu itatufanya tupotee” (5T 546).

Mambo mawili makubwa ndiyo yatakayounganisha na kuleta umoja huu wa makanisa kutoka katika tofauti zao za mafundisho. Nayo ni “Kwa njia ya makosa makuu mawili – imani kwamba roho haifi, na utakatifu wa jumapili – Shetani atawaleta watu chini ya madanganyo yake. Wakati lile la kwanza linaweka msingi wa imani ya umizimu, lile pili linaleta mapatano ya kukubaliana na Rumi” (GC 578). Mama White anakazia umoja kwa kanisa la Mungu kwa kadri tunavyofunga historia ya dunia. Anasema, “Ulimwengu wote u kinyume chetu, makanisa yanayopendelewa na watu wengi yako kinyume chetu, sheria za nchi hivi karibuni zitakuwa kinyume chetu. Kama kuna wakati ambapo watu wa Mungu walipaswa kushikamana pamoja ni sasa” (5T 236).

Tulifundishe kanisa limtambue Bwana wao aliyewaita katika wito huu mkuu. Watu wanaishi ndani ya kanisa bila kujua hatari iliyoko mbele yetu. Wanakula na kunywa, kutenda na kunena kama wadhambi wa kawaida hawajui hatari kuu iliyo mbele yetu. Mama White anasema, “Hebu walinzi sasa wapaze sauti zao na kutoa ujumbe ulio ukweli wa leo. Hebu na tuwaonyeshe watu mahali tulipofika katika historia ya unabii.” (FE 335). … Ziko nyakati za dhoruba mbele yetu, lakini hebu tusitamke neno hata moja la kutoamini au kukatisha tamaa” (ChS 136).

Tunapaswa kuzingatia kuwa wakati wa taabu uko mbele yetu, lakini hatupaswi kutoa maamuzi yatakayoleta taabu kabla ya wakati wake kwa madai kuwa tunahubiri ukweli. Ukweli ukihubiriwa ndani ya Kristo bila kutanguliza nafsi zetu, watu watamuona Kristo anayenena nao kupitia kwetu. Hivyo hawataweza kushindana nasi wala kuuzimisha ukweli. Mama White anasema kuwa: “Uko wakati wa taabu unaowajia watu wa Mungu, lakini hatupaswi kuliweka hilo mbele ya watu daima, na kuwafanya wawe na wakati wa taabu kabla ya wakati. Kutakuwa na kupepetwa miongoni mwa watu wa Mungu, lakini huo sio ukweli wa leo wa kuyapelekea makanisa yetu” (1SM 180; 2SM 13).

 

 

SOMO LA PILI.

SHERIA YA JUMAPILI MAREKANI NA ULIMWENGU KOTE.

Imeandaliwa na Mch. Filbert Joseph Mwanga

 

FUNGU KUU: UFUNUO 13:3, 8, 11 – 17.

UTANGULIZI

Pambano kuu la mwisho kati ya Kristo na Shetani, Wema na Uovu, Haki na Uasi itakuwa ni swala la Ibada. Kati ya ibada ya kweli na uongo. Wakati Adamu na Hawa walipoumbwa Mungu aliwapatia siku yake maalumu ya siku ya ibada. Siku ya Saba ya juma ilitengwa kando kwa matumizi ya pumziko takatifu, ibada takatifu, na pia fursa za pekee za kukutana na Mungu katika kutafakari kazi za uumbaji Wake.

Baada ya dhambi kuingia Shetani naye akatengeneza ibada bandia ambayo inapingana na ile ya Mungu wa Kweli. Shetani akawapatia wanadamu sabato bandia kama siku ya ibada ambayo haiwezi kuwapatia wanadamu pumziko la kweli wala ibada takatifu kwani mawazo ya watu yanakuwa yamejawa na miadi ya kuwa mara baada ya kumaliza ibada kwenda katika shughuli za maisha.

Hivyo Sabato ya Mungu (Jumamosi) na sabato bandia ya Mwanadamu (Jumapili) itakuwa ndicho kiini kikuu cha pambano kuu la mwisho. Wanadamu watapewa uchaguzi kumtii Mungu ama kumtii mwanadamu. MamaWhite anasema, “ Kulazimisha utunzaji wa Jumapili kwa upande wa makanisa ya Kiprotenstanti ni sawa na kulazimisha ibada ya upapa” (GC 448).

Jambo hili la sheria ya Jumapili ndio itaamua makundi mawili ya wanadamu: Kundi la Mungu na Kundi la Shetani. Jumapili na Jumamosi itachora mstari katika makundi haya mawili ili kuchagua watakaopokea Alama ya Mnyama na wale watakaopokea Muhuri wa Mungu. Mama White anaelezea makundi haya mawili mbele ya Maamuzi ya kila kundi kwa kusema:

“Suala la Sabato litakuwa ndilo hoja kuu katika pambano kuu la mwisho ambalo ulimwengu wote utakuwa na sehemu ya kufanya” (6T 352). … Jamii yote ya Kikristo itagawanyika katika makundi makuu mawili, wale wanaozishika amri za Mungu na imani ya Yesu, na wale wanaomsujudu mnyama na sanamu yake, na kuipokea chapa yake” (GC 450); 9T 16; 2SM 55).

Somo hili ni nyeti kulijua kwani linahusu uondolewaji wa uhuru wa dhamiri katika mioyo ya watu wa Mungu. Zaidi ya yote ni somo ambalo linagusu fahamu ya kila mwanadamu kufanya uamuzi wa makini katika maisha yake (diligently decision) kwa ajili ya wokovu wa roho yake. Ni jambo ambalo Biblia imeweka bayana katika UFUNUO 13:16 kuwa itawagusa wanadamu wote wakubwa kwa wadogo; matajiri kwa maskini; la kutisha zaidi viongozi wa wanadamu wanaofundisha maadili ya Mungu watakapomkataa Mungu na sheria yake na kukubali kuungana na ulimwengu kuwatesa watu wa Mungu. Mama White anasema,

“Waprotenstanti wa Marekani watakuwa mstari wa mbele katika kunyosha mikono yao juu ya ghuba/shimo kubwa ili kuushika mkono umizimu; watanyoosha mikono juu ya shimo kubwa lenye kilindi kirefu kushikana mikono na mamlaka ya Rumi; na ndipo chini ya uongozi wa muungano huo wa utatu, nchi hii itafuata nyayo za Rumi katika kukandamiza uhuru wa dhamiri (GC 588)…. Iwapo watu wanaweza kushawishika kupendelea iwepo sheria ya Jumapili, basi, wachungaji na mapadre wanakusudia kutumia ushawishi wao wa pamoja ili kujipatia marekebisho ya kidini katika Katiba ya nchi, na kulilazimisha taifa zima la Marekani kuitunza Jumapili” (RH Extra 24/12/1889).

SOMO

Tunapaswa kuelewa kuwa jumapili itakuwa katika awamu mbili. Awamu ya kwanza ni utangazwaji wa jumapili katika nchi ya Marekani; na awamu ya pili itakuwa ni utangazwaji wa jumapili katika ulimwengu wote. Wapo wanatheolojia wengi wanakubaliana na msimamo huu kuwa utangazwaji wa jumapili katika nchi ya Amerika itakuwa inawahusu na kuwaadhiri sana watu wa Mungu yaani wale wote ambao wamejua ukweli mapema na kwa uaminifu wanamtii Mungu na wale ambao wameujua ukweli na kucheza nao kwa muda mrefu bila kuutii.

Tunaposema Amri ya Jumapili kama alama ya mnyama maana yake nini? Hiki ni kitambulisho cha uasi wa amri ya Mungu juu ya ibada ya siku ya Saba. Muhuri wa Mungu ni ile amri ya nne inayotoa agizo la kutunza siku ya saba ya Juma yaani Jumamosi. Wakati huo huo kambi ya pili Shetani naye akaweka kitu bandia ambacho kinaonyesha alama ya utii kwake yaani sabato bandia yaani Jumapili. Mama White anasema wazi wazi kuwa,

“Hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa katika kuitukuza sabato hiyo ya sanamu, na kutaka Jumapili iadhimishwe kwa kuitungia sheria, isipokuwa Shetani ndiye amekuwa nyuma yake, na ndiye amekuwa mtendaji mkuu... Wakati Bunge litakapotunga sheria zinazoitukuza siku ya kwanza ya juma, na kuiweka mahali pa siku ya saba, hapo ndipo hila ya Shetani itakuwa imekamilika.” (7BC 977, 976).

Mama White anaendelea kusema kuwa:“Juhudi zaidi ya wazi zitafanyika ili kuitukuza sabato hiyo ya uongo, na kuonyesha dharau kwa Mungu Mwenyewe kwa kutwaa mahali pa siku ile aliyoibariki na kuitakasa… Sabato hiyo ya uongo italazamishwa kwa njia ya sheria za ukandamizaji. Shetani na malaika zake wako macho sana, nao wanashughulika kwa bidii sana, wakifanya kazi kwa nguvu na ustahimilivu kupitia kwa mawakala wa kibinadamu ili kutimiza kusudi lake la kufutilia mbali maarifa ya kumjua Mungu katika akili za watu” (RH 13/12/1892).

 

Sheria ya Jumapili Marekani

Taifa hili ambalo liliibuka kama mwanakondoo mwenye Pembe mbili (Ufunuo 13:11,12) hatimaye litanena kama joka. Mfano wa mwanakondoo ni ile hali ya Marekani ya wakati huo ilipokuwa kituo cha usalama kwa watu wa Mungu wakati wa mateso kwa kipindi cha nyuma; pia kuwa na katiba ambayo inatoa uhuru wa kuabudu kwa kila mtu bila kuingiliwa uhuru wake.

Lakini taifa hili litakapoanza kunena kama joka ni pale watakapoacha kuheshimu uhuru wa dhamiri na kulazimisha watu sheria ya kuabudu siku ya kwanza ya juma yaani JUMAPILI. Bunge la Amerika litakapotunga sheria na kuipitisha hapo ndipo taifa hili litanena kama joka (Shetani) maana yake kunena kinyume chake Aliye juu (Danieli 7:25). Mama White anasema:

“Wakati unakuja ambapo sheria ya Mungu, kwa namna ya pekee, itabatilishwa katika nchi yetu. Watawala wa taifa letu, kwa njia ya kutunga sheria Bungeni, watalazimisha sheria ya Jumapili, na kwa njia hiyo watu wa Mungu wataingia katika hatari kubwa sana. Wakati taifa letu, katika vikao vyake vya Bunge, litakapotunga sheria kuzibana dhamiri za watu kuhusiana na haki zao za kidini, likilazimisha utunzaji wa Jumapili, na kutumia Siku ya Saba, hapo ndipo sheria ya Mungu, kwa makusudi yote na nia kamili, itakuwa imebatilishwa katika nchi yetu; na uasi wa taifa utafuatiwa na maangamizi ya taifa hili” (RH 18/12/1888).

Taifa hili kubwa dunia kwa sasa litakapoamua kutupilia mbali maagizo ya Mungu halitabaki salama, bali litaanguka kama Babeli ilivyoanguka. Mama White anasema:“Wakati makanisa ya Kiprotestanti yatakapotafuta msaada kutoka kwa mamlaka za kiserikali, na hivyo kuiga mfano wa kanisa lile asi, kwa kupinga kile ambacho kwa hicho babu zao walistahimili mateso makali sana, ndipo patakuwa na uasi wa kitaifa ambao utaishia tu katika maangamizi ya taifa hili” (4SP 410 [1884]; ST 4/7/1899).

Sheria ya Jumapili kwa Ulimwengu Wote.

Amri ya jumapili katika nchi ya Marekani itakuwa imetekelezwa na bunge la nchi hii, Marekani kama polisi wa dunia yote atashawishi mataifa mengine kwa mfano wake kuanza kufuata hatua zake. Angalia swala la vyama vingi lilikuwa ni swala la nchi ya Amerika lakini hatimaye dunia nzima sasa imeingia katika mfumo huo hata kwa nchi zote za mlengo wa Mashariki yaani za ukomunisti. Jumapili katika ulimwengu ni jambo litakaloenda kwa kasi ya ajabu kama kigezo cha kuinua uchumi wa dunia na pia kuleta umoja. Biblia inasema Mnyama wa pili atatia pumzi katika sanamu ya mnyama wa kwanza ipate kunena (Ufunuo 13:14, 15).

Marekani kama nchi ya Kiprotenstanti wakiamini juu ya uwezo wa Mungu kuwa Mungu yupo pamoja nao hata kwa kuacha sheria yake takatifu, itatumia uwezo wake wa dola kulazimisha uhuru wa dhamira kwa mataifa mengine kama sehemu ya vikwazo vya kiuchumi kwa wasiokubali kutii. Mama White anasema hivi:

“Kundi lilo hilo lilitoa madai yake kwamba kuenea haraka kwa ufisadi kwa sehemu kubwa kulichangiwa na kuinajisi ile wanayoiita ‘Sabato ya Kikristo’, na kwamba kule kulazimisha utunzaji wa jumapili kungeyaboresha sana maadili ya jamii. Madai hayo yanasisitizwa hasa nchini Marekani, ambapo fundisho la Sabato ya kweli limehubiriwa kwa kiasi kikubwa” … Mataifa ya kigeni yatafuata mfano wa Marekani. Japokuwa taifa hili linaongoza, hata hivyo dhiki hiyo hiyo itawajia watu wetu katika sehemu zote za ulimwengu” (GC 587; 6T 395).

Taifa hili limekuwa na ushawishi mkubwa sana kwa dunia. Likitumia mvuto huo huo ulimwengu mzima utaingia katika taabu hiyo. Mama White anasema kuwa: “Kama ambavyo Marekani, nchi yenye uhuru wa dini, itaungana na Upapa katika kulazimisha dhamiri na kuwashurutisha watu kuiheshimu sabato ya uongo, ndivyo watu wa kila nchi ulimwenguni watakavyo ongozwa kufuata mfano wake” (6T 18).

Na hapo ndipo mahali mstari utakapokuwa umechorwa katika makundi mawili. Wakristo wa kweli na wakristo wa uongo. Wakristo ambao watasimama imara dhidi ya sheria ya Amri kumi za Mungu na Wakristo watakaofanya maridhiano ya uasi dhidi ya tabia ya Mungu. Ndipo hasira kali itakapowaka kutoka kwa waovu dhidi ya waaminifu wa Mungu. Mama White anasema,

“Amri inayolazimisha ibada ya siku hii itatangazwa ulimwenguni kote. …. Maonjo na mateso yatawajilia wale wote ambao, kwa kulitii Neno la Mungu, watakataa kuisujudu sabato hiyo ya uongo….. Ulimwengu wote utachochewa kuwa na uadui dhidi ya Waadventista Wasabato, kwa sababu hawatatoa utii wao kwa upapa, kwa njia ya kuiheshimu Jumapili, siku iliyowekwa na mamlaka hiyo ya mpinga Kristo. Ni kusudi la Shetani kusababisha wafutiliwe mbali duniani, ili kwamba mamlaka yake hapa duniani yasipate kupingwa” (7BC 976; TM 37; RH 22/8/1893).

MWITO:

Tunapaswa kuanza tangu sasa zoezi la kuwa waaminifu katika utunzaji wa Sabato ya Mungu badala ya kungojea wakati huo. Ni kwa njia ya maombi ya dhati ndio pekee yanayotupatia uzoefu wa kuwa na mafuta ya akiba wakati huo wa taabu. Mama White anasema, “Kuna watu wengi ambao wamestarehe, ambao ni kama kwamba wamelala. Wanasema, ‘iwapo unabii unatabiri kulazimishwa kwa utunzaji wa Jumapili, basi ni hakika sheria hiyo itapitishwa; na wanapokuwa wamefikia hitimisho hilo, wanakaa wakitazamia tukio hilo kwa utulivu, wakijifariji kwa wazo kuwa Mungu atawalinda watu wake wakati wa taabu. Lakini Mungu hatatuokoa ikiwa hatufanyi bidii kufanya kazi ambayo ametukabidhi” (RH Extra 24/12/1889).

Kanisa linapaswa kuamka sasa kwa usomaji wa vitabu vya Wazee na Manabii, Danieli na Ufunuo na Pambano kuu. Hivyo mwaka kesho kitabu cha mwaka ni Pambano Kuu kitakachouzwa kwa bei rahisi kwa ulimwengu mzima. Tutanunua, kusoma na kugawa kwa watu. General Conference wamepitisha mkakati huo kwa mwaka 2012. Mama White anasema kuwa: “Vitabu vya ‘Wazee na Manabii’, ‘Danieli na Ufunuo’, na ‘Pambano Kuu’ vinahitajika sana sasa kuliko wakati uliopita. Vinahitajika kutawanywa kwa wingi sana kwa sababu zile kweli zinazosisitiziwa, zitayafungua macho ya wengi yaliyopofuka. … Wengi miongoni mwa watu wetu wamekuwa vipofu kwa umuhimu wa vitabu vile hasa vinavyohitajika sana. Kama kwa busara na ustadi ungekuwa umeonyeshwa katika uuzaji wa vitabu hivi, basi, vuguvugu la sheria ya Jumapili lisingekuwa limefika hapo lilipo leo” (CM 123; RH 16/2/1905).

Kanisa ni kipindi cha mwisho tusimame imara katika kuchunguza maisha yetu na wakati huo kuwa waaminifu mbele za Mungu dhidi ya Sheria yake takatifu. Unapomwinua Yesu naye atakuinua kufanya matengenezo makubwa katika maisha yako. Maandalizi ni ya muhimu kwa kila jambo lolote duniani ili kumaliza kwa ushindi!

 

SOMO HILI LINAENDELEA MPAKA HATUA YA 7

 

Who's Online

We have 5 guests online

Morning star radio mbeya


listen with Window Media Player   listen with Winamp   listen with iTunes   listen with RealPlayer